Na edo kumwembe
Ni nchi ya ajabu kwa mwanadamu makini kuweza kuishi. Ni nchi
inayoshangaza sana, ingawa raia wake hawaonyeshi kushangazwa na matukio
kadhaa yanayotokea.
Naizungumzia Tanzania nchi niliyoishi kwa miongo kadhaa tangu nizaliwe.
Baada ya nyimbo nyingi za matatizo, dhiki, wizi, rushwa, tabu,
magonjwa na kila aina ya shida ambayo mwanadamu wa kawaida anapitia,
jawabu kubwa linapatika kwa swali; nani anajali?Ndio, nani anajali?
Hili ni swali ambalo kila Mtanzania anapaswa kuulizwa.
Ni kwa kiasi gani, mwananchi wa kawaida, kiongozi au muhusika yeyote wa
nchi hii anajali matatizo ya nchi yetu.Nimejaribu kwa kiasi kikubwa
kutazama sura za viongozi wetu, mawaziri, wabunge, Wakurugenzi, Mameneja
na kila kiongozi. Sioni anayejali.Wengi wanaongea wasichofikiria
kukifanya kwa dhati na nchi imezidi kuoza. Akili zao ziko katika wizi
kwa sababu na wananchi wenyewe wala viongozi wengine hawajali.Nchi
inatafunwa kila jua linapochomoza na kuzama. Hakuna anayejali na kila
mtu anaangalia maisha yake.
Msukuma mkokoteni haoni ni kwa namna gani anahusika na Waziri mwizi
wala Mkurugenzi wa Manispaa mla rushwa.Atajihusisha vipi? Kwa nini
atumie muda wake mwingi kujali? Kama watu wanaomzunguka hawajali kula
yake kwa nini na yeye awe anajali maisha ya wengine.Siwezi kusema
nilifaidi matunda ya utawala wa Mwalimu Nyerere. Sijui mengi
yaliyotokea wakati wa Utawala wake, lakini tangu nilipopata akili
timamu sijawahi kusikia Rais wa nchi yangu akimfukuza kazi Waziri wake
kwa rushwa wala wizi.
Je ni kweli kwamba marais wangu hawawaoni Mawaziri wezi na wala rushwa?
Kama wangekuwa watiifu na waadilifu basi nchi yetu ingekuwa mbali.
Lakini naamini wanawaona, kikubwa ni kwa vile hawajali kinachotokea.
Hawajali kwa sababu hawana sababu ya kujali. Kwa kuwa wananchi hawajali
basi na wao hawajali kama ambavyo wananchi hawajali. Wanaendelea
kutojali na daima tunaendelea kupata vizazi vya Watanzania
wasiojali.Kwani tukifungua mikataba ya ajabu ya Madini hatuwaoni
walioweka saini hizo? Tunawaona, lakini nani anajali? Nchi inasonga
mbele na maisha yanaendelea.
Huyu anajaribu kuandika gazetini kwa uchungu na yule anatamka lile
katika kipindi cha redio kwa uchungu, lakini nani anajali? Kina mama na
watoto wanafungulia michezo ya maigizo ITV na kwingineko. Nani
atawalaumu wakati watu makini wenyewe hawajali? Si afadhali nao
wasijali!Kwani yuko wapi yule Waziri aliyesema yuko tayari kuona
wananchi wanakula majani ili ndege ya Rais inunuliwe? Ndege ambayo ni
mbovu!. Si amechaguliwa tena kuwa Waziri? Nani anajali kama Rais wa
sasa hakujali? Mimi nitajali nini?
Ni mwananchi gani anajali? Walio wengi wanafanya maaandamano katika
mikasa ya kidini au ile ya kumpongeza Rais aliyefutiwa madeni ambayo
fedha zake zilitumiwa kununua mashangingi.Kuna anayejali kwenda katika
maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya umeme? Kuna anayejali
kuandamana baada ya kusikia Nesi amesababisha kichanga kufa sekunde
chache baada ya mama mjamzito kujifungua?
Hakuna anayejali kwa sababu hata akiandamana kwa uchungu mkubwa, Rais
hawezi kumwajibisha Waziri wa Afya!. Ndivyo nchi ilivyo na watu wengi
wamekwenda jela baada ya kutoa taarifa njema kwa jeshi la Polisi.
Lakini nani anajali kuwepo kwao jela? Ukitoa taarifa kuhusiana na
mkubwa fulani anayepokea rushwa, kesho yake Kamanda wa Polisi wa Mkoa
anakuonya na kukwambia uachane naye.Kwa nini niendelee kujali kwa watu
ambao hawajali? Watu wangapi walishikwa na madawa ya kulevya katika
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar es salaam lakini wapo nje kwa madai
kwamba uchunguzi unaendelea?
Uchunguzi upi wakati madawa yalitolewa tumboni na tukaonyeshwa katika
taarifa za habari za Televisheni mbalimbali? Kwa nini niendelee kujali
kuwepo nje kwa mtuhumiwa wakati Kamanda wa Polisi wa mkoa haonyeshi
kujali?Yuko wapi dada machachari Mbunge wa kike aliyedai kwamba ana
majina ya wauza madawa wa kulevya? Ni kweli kwamba alizungumza jambo
jipya katika jamii yetu ya watu wasiojali?
Tunao watu wengi wanaouza madawa na kwa bahati wanajulikana, lakini
nani anajali? Dada yule ‘alionyesha’ kujali, lakini baada ya hapo nani
amejali? Mbona hatujasikia mtu amekwenda ndani kutokana na mdomo
wake?Tangu baada ya ‘mauaji’ ya basi ya Buffalo, magari yanazidi kwenda
kasi barabarani. Nani anajali? Si mpaka watu wengine wafe ndio tusikie
tamko jingine la kinafiki?Kuna meli ngapi mbovu pale Ziwa Victoria na
sehemu nyingine zenye vyombo vya usafiri wa majini? Kwa sababu hakuna
anayekufa kwa sasa wahusika na wananchi hawajali mpaka litokee janga.
Ili mradi asubuhi inafika, mchana unapita na jioni inawadia basi hakuna
anayejali mpaka litokee janga. Nani anajali?Mchele mbovu
unahalalishwa, watu wanatengeza maji ya ‘kufoji’ na kuuza, nani
anajali? Nikienda kusema Polisi wananitazama kwa jicho la chuki lakini
tayari nimeshawaachia mianya ya rushwa.
Keshokutwa nakutana na mkubwa wa Polisi niliyemshtua akiwa pamoja na
mkuu wa Kiwanda nilichokishtaki. Wanakula ‘kitimoto’ pamoja na
wanacheka vilivyo, nani anajali?Kuna watu wachache walikiweka mikononi
Chama cha soka nchini FAT,enzi hizo. Nani alijali? Kama si kuvurugana
wenyewe kwa wenyewe wangeweza kuwepo mpaka leo.Ndio, Rais wa nchi
alikuwepo, lakini hakuwa na muda wa kujali. Kipaza sauti kilikuwa
kinamwambia asijali mambo hayo ila aelekeze macho katika Utandawazi.
Ndio, utandawazi ambao unaruhusu tupeleke makontena ya mchanga
uliochanganyika na dhahabu nje ya mipaka yetu. Nani anajali?Wachache
wanajaribu kujali lakini nani anawasikia? Wenyewe wanakutana Golden
Tulip wakila firigisi na kupeana ruhusa hizo. Mimi na wewe tujali nini
wakati hatuna uhakika wa kesho?
Tukipata watoto nao wanaingia katika mkumbo huo huo wa kutojali. Kizazi
hiki ambacho watoto wengi wamegeukia hisia za kimagharibi ni yupi kati
yao anaweza kujali?Wa kiume anakazania kusuka, wa kike anatamani kuvaa
kama Beyonce. Hakuna hata mmoja mwenye hisia na nchi. Hawezi kujali
kwa sababu hajafundishwa kujali.
Ukisikiliza maoni ya wengi kuhusiana na kesi ya Justine Kasusura, wengi
wanamlaumu kwa nini hakutoweka nje ya nchi. Hakuna anayesikitika kwa
kitendo chake cha kuiba fedha. Kwa nini?Watu hawajali alichokifanya.
Yeye alifanya hadharani lakini kuna wanaoiba kwa karatasi? Hawa akina
‘Kasusura’ wa mezani nani anawazuia? Nani anawajali?Iko wapi Kampuni ya
Richmond? Mbona kimya? Nani anajali? Kwa sasa umeme upo na watu
hawajali tena. Wanataka ije ‘Richmond’ nyingine ya Maji au huduma za
Afya. Nani anajali?
Ndio, sijawahi na wala sitaki kupiga kura. Yupo atakayesema napoteza
haki yangu ya msingi. Simuoni wa kunijali na hata kama akiamua kunijali
basi mfumo hauwezi kumsapoti anijali.Wakati wananchi wengine wakipiga
kura mimi naangalia vipindi vya soka katika Televisheni, kwa nini
uniambie sijali wakati atakayechaguliwa hatanijali?
Katika kituo cha wapiga kura chenye wakazi 1000 lakini mshindi
ameshinda kwa kura 1200, kwa nini nijali kusumbuka juani huku FFU
wakinighasi wakati waliopanga matokeo hawaijali kura yangu?Nijali nini
hasa kwa kutompigia kura mtu atakayekwenda bungeni kupitisha sheria ya
Takrima? Acha nifuatilie Ligi kuu ya England na utamu wake.
Soma magazeti yetu ya leo. Watu wameamua kuandika mambo laini ambayo si
sehemu ya mapambano yetu.Makala za leo ni zile zile zinazoelezea kwa
undani Habari za Theolojia, Ulokole, na mambo mengine. Mwananchi asiye
na uhakika na machweo ataelewa nini na kupata tumaini jema katika
makala hizi? Wanaoziandika hawajali kinachotokea kwa sasa.
Kwetu, kiongozi kutajwa anamiliki hiki na kile kwa jina la mwanae, si
kashfa. Kwetu, mtoto wa mkubwa au mkubwa mwenyewe kuua si jambo la
ajabu sana. Nani anajali? Wao na Kamanda wa Polisi wanakutana
Kilimanjaro Kempsky katika dhifa mbalimbali, unajua wanaongea nini? Kwa
nini ujitie kimbelembele cha kujali? Ili mradi unapumua, iangalie siku
yako ya kesho.Tanzania ya leo imejaa watu wanaozijali familia zao.
Nani atawalaumu watu hawa? Kwani viongozi wetu wanawajali kina nani? Si
wanajali elimu za watoto wao pale Oxford, Havard na kwingineko?Kama
unabisha, mbona sasa hivi ndio wanatuongoza? Nani anajali? Tuna uhakika
gani kama baadaye wajukuu hawataongoza? Si ndio wanapewa ukamanda wa
vijana wakijiandaa kumtawala mwanangu ambaye ni mnyonge wa baadaye? Nani
anajali?Sina hasira na mtu.
Nina furaha na maisha yangu kwa sababu napata ninachokitaka kwa
uhalali. Kama maisha yataendelea kuwa hivi basi nisilaumiwe kwa
kutojali. Nina uhakika gani kama wenzangu wanajali?Kilio kama changu
kimetamkwa mara ngapi na watu makini? Nani amejali? Kelele za mchanga
wa dhahabu nani amezijali?Waliongia mikabata mibovu ya madini nani
anawajali? Wangekuwa Chini,Japan, Uingereza na kwingineko, wangekuwa
wapi watu hawa kama si katika kuta za Gereza? Hapa kwetu nani
anajali?Lakini nijali nini zaidi wakati Rais wa nchi aliwahi kuwatamkia
watu walioelezea hisia zao kwa Waziri Mkuu wake kuhusu umilione wake
wa mashaka, kwamba wana wivu? Kama yeye mtu wa juu kabisa hakujali,
nani atajali?Utawala ule ulikumbana na migomo ya wanafunzi, huu nao
unakumbana na migomo hiyo hiyo, nani anajali? Kuna njia za kudumu za
kumaliza migomo hiyo ambayo nimeisikia tangu utotoni mwangu?Huyu
anakabiliana nayo leo, akihamishiwa anahama na hisia zake. Yule anakuja
na hisia nyingine na wala hajali kutazama alipoishia mwenzake.
Leo, kuna watu wengi wanapiga kelele kuhusiana na hatari ya kujiunga na
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nani anawasikiliza? Mimi naweza kuwa
sehemu ya maamuzi hayo?Wanaotoa tahadhari ni watu wasomi. Afadhali
ingekuwa kwangu mtu nisiye na elimu, lakini wanaotoa tahadhari hizi ni
watu wanaoheshimika kwa elimu na upeo wao.
Najua hawasikilizwi lakini nani anajali? Kama wenzao hawajali, nani
atanisikiliza mimi nisiye na lolote? Acha waamue nami nitatii kwani
waliamua mangapi ya hatari na nimeendelea kutii? SijaliLakini kwa nini
nimewang’angania wasiojali wakati hata wenyewe wakifa au kuondoka
madarakani hakuna anayewajali?
Wako wapi waliojali ambao familia zao zinaishi kama vile baba zao
hawakujali? Ndio, familia za akina Edward Sokoine. Nina uhakika watoto
wao watajuta kwa kitendo cha baba yao kujali sana wakati wa utawala
wake.Ndio, na hata ninapomaliza kuandika makala hii, wengi wataelewa
ninachomaanisha. Wakubwa wengi na watu wa kawaida wataisoma na
kuielewa. Lakini nani atajali? Posted by edo kumwembe
CHANZO:edo kumwembe
No comments:
Post a Comment