Iringa. Kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la
Kalenga zinatarajiwa kufungwa kesho huku CCM ikitarajia kumaliza kampeni
zake katika ngome ya Chadema iliyopo eneo la Kidamali.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana
anatarajia kuongoza ufungaji huo huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe akitaraji kuongoza maandamano ya kufunga mkutano wa kampeni hizo.
Katibu wa CCM mkoani hapa, Hassan Mtenga alisema
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Dk Yahya Msigwa, viongozi wa Jumuiya ya
Wazazi Taifa, Khamis Dadi (Katibu) na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo,
Abdallah Bulembo ni miongoni mwa watakashiriki kufunga kampeni hizo.
Timu ya kampeni ya CCM inaratibiwa na Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula ambaye ameweka kambi katika Kata
ya Ifunda, inayoaminika kuwa ni moja ya ngome ya Chadema .
Wengine ni Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu
Akwilombe makatibu wa CCM wa wilaya zaidi ya 10 ambao wameweka kambi
kwenye kata 13 na vijiji vilivyopo jimboni humo.
Mkutano wa Chadema unatarajiwa kufanyika katika
Kata ya Ifunda, Jimbo la Kalenga kwa mwenyekiti kuongoza maandamano
pamoja na jopo la wabunge 40 wa chama hicho. Uchaguzi mdogo wa Kalenga
unatarajiwa kufanyika Machi 16,baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa
Jimbo hilo, Marehemu Dk William Mgimwa.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian
Lubuva amevitaka vyama vya ushirika kuwarudishia shahada zao wakazi wa
Kalenga ili waweze kupiga kura.
No comments:
Post a Comment